
Meya wa Kinondoni Mh. Benjamini Sitta kulia na Meya wa Ubungo Mh. Boniface Jacob wakihesabu kura mara baada ya kura kupigwa ili kuchagua Naibu Meya wa jiji la Dar es salaam.
Hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa idadi sawa ya wajumbe kwa pande zote mbili ambapo UKAWA ulikuwa na wajumbe 12 huku CCM ikiwa na wajumbe 12.
Akizungumza wakati wakutangaza uamuzi huo ulioafikiwa na wajumbe wa baraza hilo, Mstahiki Meya Isaya Mwita amesema kuwa kutokana na hali hiyo kila mmoja ataongoza kwa kipindi cha miezi mitatu hadi Juni 30 mwaka 2019.
"Tumefikia uamuzi huo kwani viongozi wamechaguliwa kwa ajili ya kuleta maendeleo ya waanchi bila kujali vyama vyao, kuwepo kwa viongozi wa vyama viwili tofauti haitawakosesha wananchi maendeleo kwakuwa wote wamechaguliwa kwa lengo la kuwatumikia wakazi wa jijini hapa", amesema Meya Mwita.
Kabla ya kufanyika kwa maamuzi hayo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamini Sita alitoa hoja baada ya kuwepo kwa mvutano mkali kuwa baraza lijigeuze kamati ili kufanya maamuzi ambayo yatakuwa na maslahi kwa wananchi kuliko kuendelea na mabishano.
“ Ndugu mwenyekiti hakuna haja ya kuendelea kubishana, wote hapa tunafanya kazi kwa ajili ya wanachi wa jijini hapa, ningeshauri tujigeuze kamati ili kufikia muafaka wa jambo hili".
Baada ya hoja hiyo kutolewa, wajumbe wa baraza hilo walikubaliana kama kamati, ambapo baada ya nusu saa walirudi kuwa baraza na hivyo Meya Mwita kutoa maamuzi ya uchaguzi huo.
Uchaguzi huo umefanyika leo ikiwa ni baada ya aliyekuwa Naibu Meya Mussa Kafana kujiuzulu nafasi yake na kujiunga na CCM Septemba mwaka huu.