Ijumaa , 28th Sep , 2018

Kuelekea siku ya maadhimisho ya moyo duniani tarehe 29 Septemba, inadaiwa takribani watu milioni 17 hufariki kutokana na ugonjwa wa moyo kila mwaka,ambapo inakadiriwa kuwa ni 31% ya vifo vyote vya watu duniani.(kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, (WHO).

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza na www.eatv.tv Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Kuboja amesema magonjwa ya moyo yanachangia kwa kiasi kikubwa katika vifo vya watu duniani huku ya kiwashambulia watoto, watu wa umri wa kati pamoja na wazee.

Kwa watoto tatizo hili linatokana na kurithi, kuzaliwa nalo au Rheumatic fever, (homa ya riumatiki), kwa upande wa kuzaliwa takribani watoto 1000 kati ya watoto 8 mpaka 10 hufariki kutokana na magonjwa ya moyo na ile ya rheumatic fever kati ya watoto 1000 watoto 10 mpaka 20 wanaugua ugonjwa huo” _Amesema Dkt Kuboja.

Pia Dkt kuboja ametaja visababishi vinavyochangia magonjwa ya moyo kwa watu wazima kuwa ni matumizi ya pombe, kuugua kwa kisukari, kuziba kwa mishipa na damu katika moyo kutokana na kula vyakula vya mafuta, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, kutofanya mazoezi,shinikizo la damu, pamoja na unene uliokithiri.

Aidha dkt kuboja amebainisha magonjwa mbalimbali ya moyo ambayo ni pamoja na kuzaliwa kwa moyo wenye kilema, kuwa na maambukizo kutoka kwa wazazi hususani kwa watoto waliozaliwa, kuchoka kwa nyama zinazosukuma (ku-pump) damu na mengineyo.

Akizungumzia tofauti ya mshtuko wa moyo (Heart Attack) na ugonjwa wa moyo Dkt kiboja amesema,

“_kitu chochote kinachodhuru moyo kama hakikutibiwa, kinaweza kikakupatia ugonjwa wa moyo, kama haukutibiwa moyo unaweza ukachoka na ukasimama ndio tunasema heart attack”._

Kuboja ametoa wito kwa watanzania kufanya uchunguzi wa afya zao katika hospitali mbalimbali nchini ili kujikinga na maradhi yatokanayo na ugonjwa wa moyo huku akiwataka watanzania wajitokeze katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani inayoadhimishwa tarehe 29 September duniani kote, huku kitaifa yakiadhimishwa katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.