Alhamisi , 30th Aug , 2018

Kocha wa Arsenal, Unai Emery amewazuia wachezaji wake kutumia juisi ya matunda kutoka katika chakula kinacholiwa wakati wa mazoezi ikiwa ni moja ya mkakati wa kuwapa utimamu wa mwili wachezaji hao.

Wachezaji wa Arsenal wakiwa mazoezini.

Emery, ameutambulisha mkakati huo mpya baada ya kuachana na utaratibu wa awali uliokuwa ukitumika huku akiwahimiza wachezaji kutumia maji zaidi kuliko juisi hizo za matunda.

Inaelezwa kuwa mpango huo ulianza mara tu baada ya kocha huyo kupewa kibarua cha kuinoa klabu hiyo kufuatia kocha, Arsene Wenger aliyedumu klabuni hapo kwa takribani miaka 22 kustaafu mwishoni mwa msimu uliopita.

Arsene Wenger ndiye kocha aliyefahamika kwa kutilia mkazo mfumo bora wa lishe kwa wachezaji wake katika soka la kiingereza tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 1996.

Wakati alipokuwa akitambulisha mfumo huo, Wenger aliwazuia wachezaji wake dhidi ya matumizi ya vyakula kama chocolate na kupendekeza wale zaidi kuku, samaki na mboga za majani kwenye chakula chao wakati wa mazoezi ya klabu hiyo, Colney jijini London.