Jumanne , 28th Aug , 2018

Katika kuhakikisha anapandisha ufaulu kwa wanafunzi wa wilaya ya Kisarawe, Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo amekutana na makundi yote husika ambayo ni wazazi, walimu na wanafunzi na kuwambusha wajibu wao.

Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Mh. Jokate Mwegelo akiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Chanzige B.

Akiongea katika mkutano  uliofanyika kwenye Shule ya Msingi Chanzige B, wilayani humo, Jokate amewasisitiza wazazi kuwa wao ndio wenye jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanapenda shule kitu ambacho kitasaidia kuongeza ufaulu.

''Wazazi na jamii kwa ujumla mna jukumu kubwa la kuandaa watoto na vijana wetu na kuwahamasisha kupenda shule, pia kushiriki katika maendeleo yao shuleni ili tupate vijana wasomi wengi zaidi wanufaike na Tanzania ya viwanda,'' alisema Jokate

Aidha, mkuu wa wilaya huyo amewaasa wananchi kushirikiana na walimu pamoja na viongozi wao katika kutatua kero na changamoto mbalimbali kuanzia shuleni na shughuli zingine za maendeleo. 

Pia amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo, kama watumishi wa wananchi inawapasa kusikiliza watu wa rika zote wakubwa kwa wadogo, kwani uongozi shirikishi ndio msingi wa maendeleo.