Jumatatu , 21st Jul , 2014

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA imesema kuwa pamoja na serikali kusita kuweka bayana masuala yahusuyo chaguzi za serikali za Mitaa kwa lengo la kushtukiza uchaguzi huo, wao wamejiandaa kwa namna yeyote kushinda chaguzi hizo.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo - CHADEMA.

Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mhe. Freeman Mbowe wakati akitoa maazimio ya kamati kuu ya chama hicho pamoja na mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya chama hicho.

Kwa upande Mwingine Mhe.Mbowe akizungumzia mchakato wa katiba mpya amesema viongozi wa umoja wa katiba ya wananchi UKAWA bado wanaendelea na msimamo wao wa kutorejea katika bunge maalum la katiba.

Wakati huo huo, mbunge wa jimbo la Ubungo Mh. John Mnyika ameitaka serikali kupitia Wizara ya Maji kuchukua hatua ya kuwaita wakazi wa Goba jijini Dar es Salaam, kuwaeleza hatma ya kupata maji ili kuepusha hasira walizonazo wananchi hao juu ya ahadi ya kupata maji isiyotimizika.

Akiongea na East Africa Television jijini Dar es Salaam, Mh. Mnyika amesema wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanataka uhakika wa kupata maji safi, ambayo imekuwa ni kero yao ya muda mrefu sasa.