
Wachezaji wa timu ya Dream Chaser (wenye jezi nyeupe) na mchezaji wa TMT (mweye jezi ya blue) kwenye moja ya mechi za Sprite Bball Kings 2017.
Katika mechi hizo 25 za mchujo, zitahusisha timu 50 ambazo zitachuana kwaajili ya kusaka timu 15 zitakazoungana na bingwa mtetezi, Mchenga Bball Kings, kwenye hatua ya 16 bora. Kanuni za mashindano zinamruhusu bingwa mtetezi kuanzia hatua hiyo.
Kwa mujibu wa kamati ya mashindano, mechi zote 25 zitapigwa siku hiyo, kuanzia saa 2 asubuhi. Washindi 15 wenye pointi nyingi watapata nafasi ya kusonga mbele, hivyo timu zitalazimika kusaka pointi nyingi ili kujihakikishia nafasi kwenye 16 bora.
Aidha mechi hizo zitachezwa kwa kufuata mtiririko wa timu zilivyopangwa kwenye droo iliyofanyika Juni 20, 2018 kwenye ofisi za East Africa Television, ambapo mechi ya kwanza itakuwa ni kati ya Dream Chaser dhidi ya TMK Heroes.
Tayari kamati ya mashindano na timu shiriki kwa pamoja wameshakubalina juu ya kanuni mbalimbali za mashindano ikiwemo usajili wa wachezaji wasiozidi watatu kutoka daraja la kwanza pia wachezaji wote wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania.
Pia kati ya wachezaji watatu wa daraja la kwanza ni wawili tu wanatakiwa kucheza pamoja uwanjani huku mmoja akiwa nje na endapo atatakiwa kuingia, mmoja lazima atoke kumpisha mwenzake.