Jumamosi , 12th Jul , 2014

Bodi ya wakurugenzi ya Benki ya Dunia WB imeidhinisha Dola za Kimarekani milioni 112 kwa ajili ya kuisaidia Tanzania kuimarisha sekta ya Elimu kupitia Mpango wa matokeo makubwa Sasa BRN.

Benki ya Dunia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania Philippe Dongier amesema pamoja na msaada huo, Benki hiyo pia imeidhinisha msaada wa kuimarisha Sekta ya elimu ya Sayansi na Teknolojia.

Bw. Dongier amesema Benki ya Dunia imeanzisha program mpya ambayo inaangalia matokeo ya sekta ya Elimu nchini ambapo fedha hizo zitatumika kwa miaka minne kuanzia sasa.

Akizungumzia msaada huo wa kuimarisha sekta ya elimu kupitia BNR, Dongier amesema takribani muongo mmoja sasa, Zaidi ya watoto milioni moja wenye umri wa kuanza shule nchini waliandikishwa na kwamba jambo muhimu hivi sasa ni kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.

Naye mtaalamu wa Masuala ya elimu wa Benki hiyo Arun Joshi amesema kupitia program hiyo mpya ya Elimu kutoka Benki ya Dunia,Tanzania ambayo ni mshirika wake itafaidika kwa kuhakikisha watoto wa shule za msingi na Sekondari wanasoma katika mazingira bora.