Mkuu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza kufanya uchunguzi kifo cha Kaimu Balozi wa Libya, Ismail Nwairat aliyejiuwa kwa kujipiga risasi, ili kubaini chanzo cha kuchukua uamuzi huo wa kukatiza maisha yake.
Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda Maalum Suleiman Kova amesema jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa tukio hilo lililotokea juzi ambapo marehemu Nwairat alijifungia ofisini na kujifyatulia risasi kifuani upande wa kushoto na kujiua.
Kifo cha balozi Nwairat kimetokea juzi majira ya saa saba mchana ofisini kwa Kaimu Balozi huyo katika jengo la ubalozi wa Libya mtaa wa Upanga jijiniDSM. Inataarifiwa kuwa balozi Nwairat alijifungia ofisini na kujifyatulia risasi kifuani upande wa kushoto.
Kufuatia tukio hilo, maafisa ubalozi walivunja mlango waliposikia mlipuko wa bunduki na kumkuta Kaimu Balozi Nwairat ameanguka chini. Walimkimbiza hospitali ya AMI Oysterbay ambako alitangazwa kuwa alikwisha kufariki, kifo ambacho kimethibitishwa na jeshi la polisi nchini.
Wakati huo huo Kamanda Kova amesema jeshi la polisi bado linawatafuta watu wawili waliolifyatulia risasi gari la Magereza jana saa 7:50 mchana eneo la Regency karibu na kwa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuwajeruhi askari wawili wa magereza pamoja na mahabusu mmoja.
Amesema kuwa bado haijafahamika mara moja nia hasa ya watu hao kulifyatulia risasi basi hilo la mahabusu, lililokuwa likitokea Mahakama ya Mwanzo ya Kawe kwenda Mahakama ya Kinondoni kuchukua mahabusu wengine.