Jumamosi , 20th Jan , 2018

Timu ya JKT Tanzania inayofundishwa na kocha Bakari Shime imerejea Ligi Kuu soka Tanzania Bara msimu ujao baada ya ushindi wa mabao 5-1 ilioupata jana jioni dhidi ya African Lyon.

Wakiwa wamekosa msimu mmoja tu wa ligi 2017/18, JKT Tanzania zamani wakifahamika kama JKT Ruvu jana wametumia vyema uwanja wa Meja Jenerali Michael Isamuhyo uliopo Mbweni JKT hivyo kutinga rasmi kwenye ligi msimu wa 2018/19.

Baada ya ushindi wa jana, JKT Tanzania imefikisha alama 31 kwenye michezo 12 na kuendelea kuongoza Kundi A, ikifuatiwa na Friends Rangers yenye pointi 22 kwenye mechi 12.

Kundi hilo limebakiwa na mechi mbili tu hivyo kimahesabu JKT Tanzania tayari wametinga ligi kuu kwani hata wakipoteza mechi zao zote bado hakuna timu itakayowafikia.

Katika kundi hilo timu za Friends Rangers yenye pointi 22 na African Lyon yenye pointi  21 zinapambana katika mechi mbili za mwisho kuwania nafasi moja ya kupanda ligi kuu iliyobaki katika kundi hilo.