Ijumaa , 22nd Dec , 2017

Maafisa wa polisi katika mji wa kusini mwa India wa Hyderabad, wamesema, wamemkamata mwanamume mmoja baada ya mwanamke mmoja kuchomwa moto hadi kufa wakati wa mgogoro.

Polisi wamesema mwanamke huyo, Sandhya Rani, mwenye umri wa miaka 25 alikuwa anaelekea nyumbani wakati aliposhambuliwa jana na mshukiwa Karthika Vanga, ambaye ni mfanyakazi mwenzake wa zamani.

Watu hao wawili walionekana wakijibizana kabla ya mwanamume huyo kuchukua mafuta ya taa, na kumwagia mwilini na kumchoma moto ambapo inadaiwa Bw. Vanga amekuwa akitaka kumchumbia Bi Rani kwa kipindi cha miaka miwili.

Mwanamke huyo alikuwa amekataa mara kadhaa kuchumbiwa na bwana huyo ingawa polisi wanasema haijulikani iwapo kulikuwa na malalamishi dhidi ya mtu huyo.