Jumanne , 19th Dec , 2017

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli ametoa onyo kwa viongozi wa Serikali hasa anaowateua kuheshimu na kuzingatia maagizo yanayotolewa na viongozi wa chama hicho ikiwa ni pamoja na kuwajibika vinginevyo atawachukulia hatua.

Kauli hiyo ya Mwenyekiti wa CCM ilitolewa jana na Dk. Magufuli ambaye pia ni Rais wa Tanzania ambapo alisema kwamba viongozi wanapaswa kutambua kwamba waajiri wao wakuu ni serikali ya CCM.

“Viongozi wa Serikali katika ngazi yoyote watambue kuwa waajiri wetu wakuu ni CCM, mimi bila CCM nisingekuwa Rais, CCM ndiyo imejadili jina langu. Tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza ilani ya CCM na wenye ilani hiyo ni hawa wajumbe nendeni mkawasikilize. Kiongozi wa Serikali wa cheo chochote anawajibika kwa viongozi wa CCM,” ,” alisema.

Pamoja na hayo Dk. Magufuli ameonya kwamba asije kutokea kiongozi yeyote wa Serikali wa kusema hayajui mambo ya CCM.

“Kama mimi Rais niliyewateua ninayajua ya CCM asitokee mtu yoyote akasema hayajui mambo ya chama changu. Nataka pia viongozi wa CCM kuheshimu viongozi wa Serikali na viongozi wa Serikali kuheshimu sana sana sana viongozi wa chama,” alisisitiza

Jana Dkt. Magufuli alichaguliwa na wajumbe wa mkutano huo kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa muda wa miaka mitano baada ya kupigiwa kura zote 1,821.