Ijumaa , 5th Mei , 2017

Mkongwe mwenye miaka 15 kwenye  'game' ya bongo fleva,  Abubakar Katwila a.k.a 'Q chief' amedai kuwa maumivu na changamoto nyingi alizozipitia kwenye muziki ni mafanikio tosha kuliko hata nyumba na magari.

Q Chief amefunguka hayo kwenye eNEWZ ya EATV, amesema kuwa yeye ni muumini mkubwa wa kuamini katika furaha hivyo hata  kama hajapata chochote katika miaka 15 ndani ya muziki wake bado amani anayoipta akikumbuka maumivu ni ushindi mkubwa.

"Mimi ni mtu ambaye nimepitia maumivu sana kwenye huu muziki. Siwezi kusubiri eti niwe na magari au majumba ndiyo nisherehekee miaka yangu lakini mimi kuwa na amani ni kitu kikubwa sana. Napata sana furaha kuona bado nina pumzi na furaha yangu. Nafasi niliyopata naamini kuwa hivyo vitu vidogo vidogo nitavipata" - Q Chief.

Pamoja na hayo Q Chief amewataka mashabiki zake wamshike mkono ili kutimiza ndoto alizo nazo huku akisisitiza kuwa bado ana kipaji kikubwa na bado anataka kuonyesha kwa watu uwezo wake lakini haijalishi kama atapata mafanikio au la.

"Haijalishi nimeanguka mara ngapi, cha msingi ni kwamba nimekubali kuwa nilianguka na nimeinuka nikiwa jasiri, Nina kipaji kikubwa sana ila nataka mnishike mkono kuninyanyua zaidi ili niweze kupata mafanikio mnayotaka niwe nayo. Nafasi ya kupata vitu vizuri na vikubwa ninayo kwa sababu natafuta, lakini nisipopata pia siwezi kuwa na tatizo"- Q Chief.