Jumatatu , 6th Mar , 2017

Baada ya kuichapa Stand United mabao 2-0 juzi usiku, sasa Klabu ya Azam FC, imehamishia vita yake katika mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland.

Azam FC Vs Stand United katika dimba la Chamazi

Mchezo huo wa awali wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo, utafanyika ndani ya Uwanja wa Azam Complex Jumapili ijayo Machi 12 kabla ya kurudiana jijini Mbabane, Swaziland katika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo Machi 19.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aristica Cioaba, alisema kuwa mchezo huo ni muhimu sana kwao na kwa sasa wametilia mkazo kuandaa programu ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Mbabane.

Cioaba, amesema kuwa kuanzia wiki ijayo anataka kumuona kila mchezaji wake akiwa tayari kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya Mbabane, ambayo inakutana na Azam FC baada ya kuitoa Orapa United ya Botswana kwa jumla ya mikwaju ya penalti 3-2 kufuatia sare ya bao 1-1

“Ninachowahidi mashabiki wa Azam FC itakuwa ni moja ya mechi nzuri, kila mchezaji analitambua hilo kuhusu mechi hii na kwa uhakika wataingia uwanjani kucheza vizuri na kupata matokeo mazuri, ninaiamini timu yangu kuelekea mchezo huo,” alisema.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya aina yake ya kucheza jumla ya mechi 15 mfululizo mwaka huu bila kupoteza hata moja huku ikiwa imeruhusu wavu wake kuguswa mara moja tu.