Charles Mkumbo - Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema chanzo cha mauaji hayo ni wafugaji wa kimaasai kuwavamia askari hao ambao walikuwa wamekamata ng’ombe ambao waliingizwa ndani ya msitu wa hifadhi ambao ni wa serikali, kwa ajili ya malisho, kutokana na ukosefu wa malisho.
Kamanda, Mkumbo,amesema Askari hao ambao wanalinda msitu huo maarufu , shamba la miti la Meru USA Plant ,ambalo ni la serikali, walianza oparesheni zao majira ya saa 2.30 asubuhi za kuondoa mifugo iliyoingizwa ndani ya msitu huo.
Askari hao wa SUMA JKT, awali walikamata ng’ombe 45 , mbuzi na kondoo 65 na kuwapeleka kwenye zizi maalumu lililopo kituo cha polisi Oldonyo Sambu.
Askari hao waliendelea na oparesheni hiyo na ilipofika majira ya saa 8 mchana walipata taarifa ya kuwepo kwa kundi jingine katika msitu huo na kufanikiwa kukamata ng’ombe 80, mbuzi na kondoo 70 kwa lengo la kuwapeleka kwenye zizi hilo la serikali.
Amesema wakati wanawaswaga mifugo hao ndipo kundi la wananchi wakiwa na silaha za jadi walipojitokeza mbele yao wakitaka kuwakomboa mifugo hao kwa nguvu.
Hatua hiyo iliwalazimu askari nao kuanza kuwafyatulia risasi na kusababisha vifo vya vijana wanne na watano kujeruhiwa.
Amewataja wananchi waliouawa kuwa ni Mbayan Melau (27), Julius Kilusu (45), Lalasehe Meibuko (25), na Seuri Malita (32) na hakuna askari aliyejeruhiwa.
Diwani wa kata ya Oldonyo Sambu, Raymond Lairumbe amesema hatazika miili hiyo, mpaka viongozi wa serikali watakapofika eneo hilo kuzungumza nao na huku majeruhi wanne waliolazwa hospitali ya Mount Meru Arusha, wakiomba msaada wa kutolewa risasi katika miili yao.