Jumatano , 16th Nov , 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema serikali inakusudia kuboresha usafirishaji kwa njia ya reli ikiwa ni pamoja na kuunganisha Mkoa wa Dodoma na Dar es salaam ambapo watu watatumia masaa 3 pekee kutoka mikoa hiyo.

Prof. Makame Mbarawa

Akitoa hotuba mara baada ya kuzindua bodi mpya ya Kampuni za Reli Tanzania TRL Jijini Dar es salaam, Prof Mbarwa amesema kwa sasa wanalenga kufikia usafirishaji wa mizigo kwa kiwango cha tani 100 ambapo ameitaka bodi hiyo kuhakikisha kuwa inaendeleza mikakati yote ya shirika hilo na kujiendesha kibiashara.

Naye Msajili wa Hazina Florence Mafuru amesema, kwa muda mrefu sasa shirika la reli TRL inajiendesha kwa hasara na kuipatia serikali mzigo mkubwa wa kuihudumia shirika hilo ambapo amewataka wajumbe wa bodi hiyo mpya kuhakikisha kuwa wanashugulikia changamoto zote za kiutendaji ili kufikia kiwango cha kuchangia asilimi 15 ya pato la taifa.

Lawrence Mafuru - Msajili wa Hazina

“TRL inaendeshwa kwa hasara jitihada za kulifufua ziendane na mbinu za kisasa za kibiashara, nafanya mazungumzo na wataalam wa kibiashara wawaambie ni namna gani itaweza kujiendesha kwa faida na kuepuka mianya yote inayoliingizia hasara TRL” Amesema Lawrence

Aidha, amebainisha kuwa kwa muda ambao shirika hilo lilianzishwa ilipaswa kuwa na uwezo wa kuwekeza katika nchi za jirani kama yafanyavyo makampuni na mashirika ya nchi zingine na kwamba kwa sasa wawe na mikakati ya kujiendesha kimataifa.

“Kwanini isitokee shirika la serikali kuwekeza hadi nje ya nchi? Makampuni mengi ya nje yameweza kuwekeza hapa, ningependa kuona shirika hili linafikia huko ili kukuza uchumi wa nchi yetu na kukuza ajira” amesema.