Jumatatu , 14th Nov , 2016

Serikali inaendelea na mazungumzo kuona ni kwa kiasi gani inaweza kupunguza kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 18 ili kiendane na kile kinachotozwa na nchi za jirani kama Kenya na Ethiopia.

Bw. Clifford Tandari

 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Bw. Clifford Tandari amesema hayo katika mkutano baina ya serikali na wawekezaji kutoka nchini Ubelgiji, ambao wapo nchini kuangalia fursa uwekezaji kwenye sekta za kilimo na usafirishaji.

Kwa mujibu wa Bw. Tandari, lengo la kufanya mapitio ya kodi hiyo ni kutokana na uwepo wa dhana kwamba Tanzania ndiyo nchi inayotoza kiwango kikubwa cha kodi ya ongezeko la thamani ikilinganishwa na majirani zake na kwamba hicho kinawezaa kuwa kigezo na sababu ya wawekezaji kuogopa kuja kuwekeza nchini.

Kuhusu ujio wa wawekezaji kutoka nchini Ubelgiji, Bw. Tandari amesema Tanzania itanufaika na uongezaji thamani utakaofanywa na wawekezaji hao kutokana na teknolojia kubwa waliyonayo kwenye maeneo wanayotaka na kuja kuwekeza na hasa kipindi hiki ambapo mkazo wa serikali ni katika matumizi ya bidhaa zilizotengenezwa hapa hapa nchini.