Sima na Yanga
Katika mchezo huo timu ya Yanga ndiyo wamekuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa mshambuliaji Amis Tambwe dakika ya 27 ya mchezo na kuwanyanyua mashabiki wa timu ya Yanga ambao wamefurika katika kucheki mtanange huo.
Baada ya goli la Yanga mchezo huo umekubwa na vurugu kubwa iliyotokana na utata wa goli baada ya kuonenaka kwamba mchezaji Amis Tambwe aliucheza kwa mkono mpira huo kabla hajapiga shuti lililozaa goli la kwanza la mchezo huo.
Kufuatia hali hiyo mashabiki wa Simba baadhi yao walichomoa viti na kuanza kuvirusha hovyo uwanjani huku jeshi la polisi likilazimika kupiga mabomu ya machozi na kusababisha dakika kadhaa za mchezo huo kusimama.
Kufuatia kulalamikia goli hilo kati ya wachezaji wa Simba na mwamuzi Martin Sanya ambaye ndiye mwamuzi wa kati wa mchezo huo, mwamuzi amelazimika kumtoa nje mchezaji wa Simba ambaye ndiye nahodha Jonas Mkude na kufanya Simba kucheza pungufu .
Kipindi cha pili kimeanza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu Simba wakitaka kurejesha goli huku Yanga wakitaka kuongeza goli huku walimu wa pande zote wakifanya mabadiliko ya wachezaji ili kuongeza nguvu.
Dakika ya 86 ya mchezo mchezaji wa Simba Shiza Kichuya amewanyanyua mashabiki wa Simba waliokuwa wameanza kukata tama kwa kutundika goli maridadi lililotokana na mpira wa kona alioupiga ukaenda moja kwa moja kwenye nyavu za goli la Yanga na kumwacha goli kipa akiwa anashangaa kilichotokea.
Hadi filimbi ya mwamuzi Martin Sanya inalia Simba 1 Yanga 1, mchezo huo umehudhuriwa na maelfu ya mashabiki pamoja na watu mbalimbali mshauhuri kama Waziri wa Michezo Nape Nnauye, Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, msanii Mwana Fa pamoja na Ommy Dimpoz
Kufuatia matokeo hayo Simba itaendela kushikilia msimamo wa Ligi kuu Tanzania bara kwa kuwa na alama 17 kwa kucheza mechi 7 huku Yanga ikishikilia nafsi ya tatu ikiwa na alama 11 kwa kucheza mechi 6.
![](http://eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/2016/10/01/ukasha 20160808_191307.jpg?itok=sPGlwdIg)