Jame Mbatia (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda UKAWA katika mkutano na wanahabari leo.
Akitangaza uamuzi huo kwa niaba ya vyama hivyo ambavyo ni CHADEMA, CUF, ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mhe. James Mbatia amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kikao chao na viongozi wa dini kilichofanyika hapo jana.
“Mbali na kutoa mapendekezo yetu kwa viongozi wa dini juu ya sakata hili, lakini nao walituma mapendekezo kadhaa hivyo tumeamua kufuata yale waliyotuelekeza na tutarejea Bungeni kwa busara zao,” Amesema Mhe. Mbatia.
Kwa upande mwingine Mhe. James Mbatia ameitaka serikali ya awamu ya tano kupeleka muswada katika bunge lijalo la Katiba ili kufanyiwa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa.
"Endapo uhuru wa vyama vya siasa hata kwa mambo ambayo yanaruhusiwa kikatiba haupo kwa nini tuendelee kuwa na vyama vya siasa nchini ambavyo hata vikao vyake vya ndani haviruhusiwi," alihoji Mhe. Mbatia na kuongeza “Vyama vyote vifutwe ikiwemo CCM tuende vijijini kwetu au tuendelee na shuguli nyingine hii itatupa kufahamu kuwa tuna taifa la kifalme na tutashindwa kuhoji".
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA kwa upande wa Zanzibar Bw. Saidi Issa Mohamed amesema katika kikao hicho pia wamewakabidhi viongozi wa dini mapendekezo yao ambayo wamewataka wayafikishe kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli
“Viongozi wa dini wamwambie Rais juu ya yale tunayohitaji yafuatwe ili kuleta maridhiano na siyo kuwepo mvutano usio na suluhu,” alisema Bw. Mohamed.