
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani DCP Mohamed Mpinga
Kamanda Mpinga ameyasema hayo katika mahojiano maalumu katika kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na kituo cha ITV ambapo Kamanda amebainisha kwamba hadi sasa amekamatwa dereva mmoja huku mwingine akisakwa.
''Ajali ya dakawa Morogoro iliyosababisha vifo vya watu 11, ukiangalia ajali ya Singida ni uzembe mkubwa kwani inasemekana madereva wa City Boy walikuwa wanasalimiana kwa kuwashiana taa na baada ya hapo wanahama barabara na kusababisha vifo vya watu 30 na wengine kujeruhiwa, jambo ambalo ni kinyume na sheria za usalama barabarani ambapo dereva wa City Boy tayari amepelekwa mahakamani na kusomewa shitaka la mauaji bila kukusudia''amesema Kamanda Mpinga
Kamanda ameongeza kuwa ''Yapo mapungufu katika sheria zetu ambapo makosa mengine ambayo madereva wamesababisha vifo mara nyingi hutozwa faini na kifungo ni mara chache sana , ila kwa ajali ya Singida dereva mmoja tumempata na tumempeleka mahakamani kwa kosa la kuua bila kukusudia kwa kuwa kitendo alichofanya alijua nini kingeweza kutokea.''
Kuhusu takwimu za ajali Kamanda amesema kuanzia kipindi cha wiki tatu tarehe 20 Juni hadi tarehe 10 Julai tumeona matukio mengi na zimetokea ajali mbaya kuna ajali 234 na zimesababisha vifo vya watu 211 na majeruhi 379 , ukipiga mahgesabu kwa wiki tatu inaonyesha tulikuwa tunapoteza watu 10 kila siku, jambo hili limetusikitisha sana na sisi tumeendelea kujipanga kukomesha hali hii.
Katika kukabiliana na ajali Kamanda amesema yapo mapendekezo ambayo tumependekeza ambayo yanafanyiwa kazi na wadau ili kuboresha sheria na adhabu kwa wanaofanya makosa, pia tutaanza hivi karibuni kutoa pointi wakati wa uendeshaji ambapo kila atakayefanya makosa atatolewa pointi tano na akiendelea atanyang'anywa leseni na tunapoanza utekelezaji wa hili madereva wazembe wengi tutawanyang'anya leseni.
Aidha Kamanda Mpinga amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kuacha tabia ya kuwapa madereva wao fedha kwa ajili ya kulipa faini jambo ambalo linasababisha madereva hao kuwa wazembe, pia wamiliki wametakiwa kutengeneza vyombo vyao na kuhakikisha madereva wao wanakuwa na mikataba ya kazi.