Jumanne , 7th Jun , 2016

Msanii Godfrey Tumain au Dudubaya amesema lebo nyingi za muziki zinafeli kwenye muziki kutokana na wasanii waliopo hawana uelewa juu ya kazi yao ya muziki.

Dudubaya ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kuwa kutokana na kutokuwa na uelewa huo, huwapelekea wasanii kusaini mikataba, na baadaye wakishapata umaarufu hubadilika na kuleta migogoro.

“Kuna watu wengi wamekata tamaa kwa sababu wasanii wengi wa Tanzania hawana uelewa na kazi ya muziki wao, wao wanatamani kwamba hata ukimwambia utachukua asilimia 1 wanasaini mkataba bila hata kuuelewa, sasa akishapata umaarufu anaanza kubadilika, baadaye sasa ishu zinavyoenda utasikia maugomvi, na ndio maana hakuna nchi yenye maugomvi kila siku kwenye redio na Tv kama Tanzania”, alisema Dudubaya.

Pia Dudubaya amesema hana wasi wasi juu ya kuongezeka kwa lebo nyingi za muziki ikiwemo na ile ya WCB, na kusema kuwa hana wasi wasi na lebo hiyo isipokuwa ana wasi wasi na wasanii waliopo kwenye lebo hiyo.

“Kuanzisha lebo tatizo kubwa lipo kwa wasanii sio watu wenye lebo, sina wasi wasi na WCB, lakini hao wasanii nina wasi wasi nao kwamba wanaposaini hawaangalii”, alisema Dudubaya.