Jumatatu , 30th Mei , 2016

Mbunge wa Mwibara Kangi Lugola CCM amesema kitendo cha wanafunzi zaidi ya 7000 kufukuzwa Chuo Kikuu cha Dodoma na kupewa saa 24 kuondoka chuoni hapo kwa makosa yasiyo yao ni kuwafanya wanafunzi hao wakimbizi ndani ya taifa lao.

Lugola ameyasema hayo nje ya ukumbi wa Bunge mara baada ya Naibu Spika Tulia Ackson Mwansasu kusitisha shughuli za Bunge baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari kushinikiza Bunge lisitishe shughuli zake ili kujadili hoja ya dharura ya wanafunzi hao kufukuzwa bila kupewa nauli na usafiri.

''Watoto hawa hawana makosa wengine wanatoka Ngara, Lindi, Musoma wengine Arusha wanafukuzwa kwa kuambiwa ndani ya saa 24 waondoke chuoni na kupelekewa askari na mbwa, na kujaa stendi ya mabasi bila kuwa na sehemu za kujihifadhi ni kuwafanya wakimbizi ndani ya taifa lao tena wakimbizi huondolewa kwa utaratibu''-Amesema Lugola.

''Mimi kama Mbunge wa CCM mwongozo ulioombwa na Nassari kujadili jambo muhimu na kukataliwa na Naibu Spika mimi skubaliani nao kwa sababu hatujui wanafunzi hao usalama wao kwa sasa upo vipi ni lazima shughuli nyingine zisimame ili tujadili suala hili''Amesisitiza Lugola.

Aidha Mbunge wa Nyamagana Stanslaus Mabula amesema kwamba kitendo cha kufukuzwa kwa wanafunzi hao hawakutendewa haki hata kidogo na Naibu Spika hajafanya vyema kukataa mjadala huo Bungeni.

Wanafunzi zaidi ya 7000 ambao wanasoma Astashahada ya masomo ya sayansi walitakiwa kuondoka ndani ya saa 24 chuoni Dodoma kufuatia kutofundishwa kwa muda ili Chuo Kitatue tatizo hilo na kuwaita upya.