Jumatatu , 30th Mei , 2016

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Ackson, amelazimika kusitisha shughuli za Bunge baada ya wabunge kutoa hoja na kushinikiza kujadiliwa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma 7802 kufukuzwa masomo.

Bunge limesitishwa baada ya kutoelewana kati ya wabunge na Naibu Spika baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki akitanguliwa na Mbunge wa Chemba Juma Nkamia kushinikiza Bunge liahirishe shughuli zake zote zilizopangwa ili kujadili suala la zarura la wanafunzi hao kufukuzwa kwa makosa ya serikali na kupewa masaa 24 kuondoka chuoni bila kupewa nauli.

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari amesema''Wabunge wengi hasa wa upinzani jana hatujalala kwa sasabu tumekesha stendi ya mabasi Dodoma kwa sababu wananchi wamepiga simu pamoja na wanafunzi, wanafunzi wamefukuzwa siku ya jumapili, wengi wamekosa usafiri kwa kupewa saa 24 kuondoka chuoni kwa sababu serikali imeshindwa kulipa wahadhiri''

''Dodoma ni mji mdogo ambao hauwezi kuhimili wanafunzi wote hao kwa siku moja ambapo makosa siyo ya kwao, makosa ni ya serikali ambayo iliwaleta kwa 'special programe' katika serikali ya awamu ya nne, kwa ajili ya kutatua matatizo ya elimu katika shule za serikali sasa naibu Spika tena mwanamke anakataa tusijadili jambo hili wakati wanafunzi wa kike 4000 usiku mmoja wapo hawali , hawanywi, hawana pakukaa watoto hawa wa maskini wanaweza kubakwa''- Amesisitiza Nassari.

Kufuatia hoja hiyo ambayo imeungwa mkono na upinzani na baadhi ya wabunge wa chama tawala Naibu Spika kwa mujibu wa kanuni akakataa kwamba jambo hilo si la dharura na kutaka shughuli ziendelee kama kawaida jambo ambalo limesababisha malumbano ndipo kiti kikaamua shughuli kusitishwa.

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke chuoni hapo mara moja kutokana na matatizo yaliyopo katika ufundishaji wa stashahada hiyo.