Jumatatu , 9th Mei , 2016

Wadau nchini wameashauriwa kuwekeza katika Maporomoko ya Mto Luhuji yaliyopo mjini Njombe ili kuwezesha eneo hilo kuwa kivutio cha utalii.

Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji (TAJATI) Ulimboka Mwakilili.

Wito huo umetolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania (TAJATI) wakati walipotembelea kivutio hicho na kujionea madhari ya kuvutia yaliyopo katika maporomoko hayo yaliyopo pembezoni mwa mji wa Njombe.

Pamoja na mandhari nzuri ya Maporomoko hayo, mazingira hayajaboresha ambapo baadhi ya watu wanatumia vichaka vilivyopo jirani kama vyoo huku wengine wakitumia sehemu ya maporomoko hayo kusafishia Pikipiki na Baiskeli zao.

Mwenyekiti wa TAJATI Ulimboka Mwakilili, amesema ipo haja ya wadau kwa kushirikiana na serikali mkoani hapa kuboresha kivutio hicho ili kiweze kuwa sehemu ya mapumziko ya wageni na wenyeji mjini hapa.

Mwakilili amesema kwa kuboreshwa kivutio hicho serikali pia itaweza kujipatia kodi kutokana na watalii wa ndani na nje watakaofika kwenye maporomoko na kulipia kiasi cha fedha kwaajili ya utalii wa eneo hilo.

Mmoja wa wanahabari mkoani Njombe Mercy Sikabogo amesema wanahabari wana jukumu kubwa pia la kuihamasisha jamii kulitunza eneo hilo ambalo ni urithi wa kipekee kwa wakazi wa mji wa Njombe na mkoa kwa ujumla.