Jumatano , 23rd Mar , 2016

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji – PIC wameitaka Bodi ya Tumbaku nchini kuacha mara moja matumizi ya dola katika ununuzi wa pembejeo pamoja na malipo kwa wakulina.

Mbunge wa Mbeya Vijijini Bw. Oran Njeza akiwa katika moja ya shughuli zake za ukulima.
Mbunge huyo ni mtaalamu wa kimataifa wa masuala ya benki na pia ni mfanyabiashara aliyewekeza kwenye shughuli za kilimo.

Kwa mujibu wa wajumbe hao, kitendo hicho kinachofanywa na makampuni yanayonunua tumbaku na yale yanayouza pembejeo za kilimo hakikubaliki na badala yake yafuate sheria za nchi kwa kufanya malipo yote kwa fedha za Kitanzania.

Agizo hilo la Kamati ya Uwekezaji limetolewa jijini Dar es Salaam leo baada ya wajumbe wa bodi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw. Saidi Nkumba, kutetea matumizi ya katika mnyororo mzima wa kilimo na biashara ya tumbaku, kwa madai kuwa hatua hiyo inamlinda mkulima dhidi ya hasara anayoweza kuipata pale thamani ya shilingi inapoporomoka.

Katika maelezo yake, Bw. Nkumba amesema utaratibu wa malipo kwa dola umekuwa na manufaa kwa wakulima ingawa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitumia udhaifu wa utaalamu wa masuala ya kifedha kwa kuwaibia wakulima.

Wakizungumza kwa hisia, wabunge hao akiwemo mbunge wa Tunduma Bw. Frank George Mwakatuka na mwenzake wa Mbeya Vijijini Oran Njeza, wamekieleza kitendo hicho kuwa ni wizi wa wazi wazi kwa wakulima na kuitaka bodi hiyo kufuata sheria za nchi zinazokataza matumizi ya fedha za kigeni katika mzunguko wa ndani wa malipo yakiwemo ya ununuzi wa pembejeo na malipo ya mazao.

Aidha, Mbunge wa Sikonge Bw. Joseph George Kakunda amependekeza vibali vyote vya bei ya ununuzi wa mazao hususani la Tumbaku vitolewe na wakuu wa wilaya kwa madai kuwa utaratibu wa sasa ambapo maofisa ushirika wa halmashauri ndiyo wanaoidhinisha bei na mfumo wa malipo umekuwa ukitumiwa kwa maslahi binafsi ya wafanyabiashara na maofisa hao.