
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya kikao na mkuu huyo wa nchi,Rais Msaafu Benjamin Mkapa amesema lengo kubwa la kwenda kumuona Rais Magufuli ni kumpongeza kwa kupewa ridhaa ya watanzania kuongoza nchi, lakini pia kumpa salamu za mwaka mpya 2016. Pia Rais Mstaafu Mkapa amemuhakikishia Rais Magufuli ushirikiano uliotukuka na kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo.
Kwa upande wake Jaji Mstaafu Joseph Warioba pamoja na kumtakia kheri ya mwaka mpya amempongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyoanza kazi vizuri kwa kukusanya mapato ya nchi kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu yanayowahusu wananchi yakiwemo afya na maji.
Jaji warioba amewaasa watu wote kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya ya kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, na wizi wa mali ya umma.
Aidha ziara ya viongozi hawa wastaafu ni mwendelezo wa Rais Magufuli kutembelewa na viongozi mbalimbali wastaafu wa serikali, dini, na vyama vya kisiasa huku pia nchi zenye uwakilishi hapa nchini zikifanya hivyo hivyo lengo likiwa ni kumuunga mkono katika mabadiliko ambayo anayafanya katika ngazi mbalimbali hususani kuwatimua kazi wazembe na wahujumu uchumi.
