Alhamisi , 17th Dec , 2015

Kiungo wa klabu ya Azam ambaye anakipiga kwa mkopo ndani ya Mtibwa Sugar Kelvin Friday ameungana na wenzake jijini Mbeya tayari kuanza kuitumikia klabu yake hiyo mpya kwa mechi ya ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya wenyeji wao Tanzania Prisons jumamosi.

Kelvin Friday akiwa katika jukumu la timu ya Taifa lakini kwa sasa ametua kwa mkopo ndani ya wakatamiwa wa Mtibwa Sugar licha ya kuhusishwa kwake na kuhitajika nchini Ethiopia katika timu ya St George.

Akizungumza na East Sfrica Radio msemaji wa wakatamiwa hao Thobius Kifaru Ligalambwike amesema nyota huyo ameongeza upana katika kikosi chao ambacho kimepania kurejesha heshima waliyoiweka msimu wa mwaka 1999-2000 walipotwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo.

Kifaru amesema waliamua kumtwaa nyota huyo pamoja na Boniface Mganga aliyekuwa akikipiga na Simba katika dirisha dogo la usajili lililofungwa desemba 15 mwaka huu ili kuhakikisha wanaendeleza kasi yao waliyoanza nayo msimu huu.

Mtibwa Sugar ilishindwa kutamba kwenye mechi iliyopita walipopoteza uongozi wa bao 2-0 mbele ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuruhusu bao zote kusawazishwa na kuambulia pointi moja kwenye mechi hiyo.