
Wananchi wakiwa katika Foleni ya kuingia kupiga kura katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25,mwaka huu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania NEC imetangaza kufanyika kwa uchaguzi siku ya kesho Novemba 22, katika majimbo mawili na kata sita ambazo uchaguzi wake uliahirishwa kutokana na vifo vya wagombea.
Vifo vya wagombea vilivyosababisha uchaguzi katika majimbo haya kuahirishwa ni pamoja na kifo cha aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Ulanga Mashariki kupitia CCM na Waziri wa Utumishi Celina Kombani, pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Lusoto kupitia CHADEMA, Mohamed Mtoi waliofariki wakati wa kipindi cha kampeni.
Kaimu mkurugenzi wa NEC Bw. Emmanuel Kawishe amesema uchaguzi huo utaanza kesho na utashirikisha majimbo ya Lushoto na Ulanga Mashariki huku kata zikiwa ni zile za Muleba, Uyole, Bukene, Msingi, Bomang'ombe, na Kasulu.
Bw. Kawishe ametoa wito kwa wananchi wa majimbo husika na kata husika kujitokeza kwenye vituo walivyojiandikisha ili kuweza kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.
Katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Lulindi ambao ulifanyika Novemba 15, mwitikio wa wananchi katika jimbo hilo ulikuwa ni mdogo ambapo ni takriban asilimia 30 pekee ya waliojiandikisha, ndiyo waliopiga kura wengi wao wakiwa watu wazima, tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.