Ijumaa , 6th Nov , 2015

Saa chache baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameanza kazi kwa kasi ambapo ameanza kazi kwa kumteua mwanasheria mkuu na kuitisha bunge.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa rais Bi. Samia Hassan Suluhu

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kuwa Rais Magufuli ameanza kazi jana kwa kumteua mwanasheria mkuu wa serikali ambaye ni George Mcheche Masaju aliyewahi kushikilia wadhifa huoo, katika serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Rais mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Mwanasheria huyo mteule ameapishwa leo saa nne asubuhi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Aidha Balozi Sefue ameeleza kuwa Rais Magufuli ameitisha Bunge la 11 ambalo litafunguliwa rasmi tarehe 17/11/2015 na kuongeza kuwa huenda mpaka kufikia tarehe 19 mwezi huu Rais atakuwa amependekeza jina la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa serikali ya awamu ya tano na kusubiri ridhaa ya wabunge.