Jumatano , 16th Sep , 2015

Chama cha waandishi wa Habari za Michezo nchini TASWA kinatarajia kutoa tuzo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na wana michezo 10 waliofanya vizuri zaidi ndani ya miaka 10 ya Rais wa Tanzania.

Mwenyekiti wa TASWA Juma Pinto amesema hafla hiyo inayotarajiwa kufanyika Oktoba nane mwaka huu ni maalumu kwa ajili ya kumuaga Rais Kikwete ambaye anamaliza muda wake kikatiba ambapo TASWA itakabidhi tuzo maalumu kwa Rais, ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa maendeleo ya michezo wakati wa miaka 10 ya uongozi wake.

Pinto amesema, TASWA imeona kuna haja ya wanamichezo kuagana na Rais Kikwete na kumpa tuzo kutokana na masuala mbalimbali aliyofanya kwa miaka yake 10 katika kusaidia kukuza michezo na sanaa nchini.

Akitoa mfano wa mambo hayo Pinto amesema kuwa ni pamoja na serikali kulipia makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi na pia serikali ilipeleka wanariadha China, Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kurejesha michezo shuleni pamoja na mashindano ya michezo kwa shule za msingi na sekondari UMITASHUMTA na UMISSETA.