Jumatano , 16th Sep , 2015

Wakulima wengi nchini wanalazimika kuuza mazao yao kwa bei chini pale wanapougua ili kupata fedha za matibabu na hivyo kuendelea kuwa na hali duni ya maisha, changamoto ambayo inaweza kuondolewa kwa kuhamasisha wakulima kujiunga na mfuko wa taifa.

Wakulima wakiwa Shambani wakiangalia Ustawi wa Mazao yao

Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Ihanda wilayani Mbozi wamesema kuwa hulazimika kuuza sehemu kubwa ya mazao yao kwa bei ya chini pale inapotokea mwanafamilia ameugua ili kupata fedha za matibabu, hali ambayo inawadidimiza kiuchumi na kuendelea kuwafanya masikini.

Afisa matekelezo wa mfuko wa taifa wa bima ya afya mkoa wa Mbeya, Paulo Bulolo amesema changamoto hiyo imepatiwa ufumbuzi na mfuko wa taifa wa bima ya afya kwa kuanzisha mpango ujulikanao kama kikoa ambao unawaelekeza wananchi kujiunga kwenye vikundi na kisha kuingizwa kwenye mfuko huo kwa ajili ya kujipatia huduma za matibabu.

kwa mujibu wa mpango wa kimkoa, mwananchi ambaye amejiunga katika vikundi anapaswa kutoa shilingi 76,800 pekee kama kiingilio kwenye mfuko wa taifa wa bima ya afya na hivyo kupata huduma za matibabu katika hospitali zote ambazo zimesajiliwa na mfuko huo nchini katika kipindi cha mwaka mmoja.