Alhamisi , 3rd Sep , 2015

Timu ya Taifa ya Tanzania yenye wachezaji wapatao 30 na viongozi 7 wa michezo mbalimbali inatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam leo jioni na ndege maalum kuelekea Congo Brazaville kushiriki katika michezo ya Afrika (All Africa Games).

Mkurugenzi Idara ya Habari, Assah Mwambene amesema Tanzania itawakilishwa na michezo sita ikiwemo mchezo wa Ngumi za Ridhaa yenye wachezaji watatu, Timu ya Mpira wa Miguu ya wanawake (Twiga Stars) yenye wachezaji 18, na Timu ya Riadha yenye wachezaji wanne, timu ya kuogelea yenye wachezaji wawili, wachezaji wawili wa Judo pamoja na michezo kwa watu wenye ulemavu yenye wachezaji wawili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Michezo, Juliana Yassoda amesema Timu ya Taifa ya Tanzania ilikuwa iondoke kwenda Congo Brazzaville hapo jana lakini kutokana na ugumu wa upatikanaji wa nafasi katika ndege mbalimbali timu hiyo imelazimika kuondoka leo na usafiri maalum.

Michezo ya Afrika inaanza kutimua vumbi hii leo ambapo Twiga Stars itafungua dimba na Ivory Coast Septemba 6, kabla ya kumenyana na Nigeria Septemba 9 na kumaliza mechi za kundi lake kwa kumenyana na wenyeji Kongo-Brazzavile Septemba 12 ambapo timu mbili kutoka kundi A zitaungana na timu mbili nyingine kutoka kundi B kucheza hatua ya nusu fainali.