Alhamisi , 16th Jul , 2015

MKUU wa Mkoa wa Arusha Daud Ntibenda, amewataka wakazi wa Arusha waliokuwa bado kujiandikisha katika daftari la mpiga kura, kwa kutumia mfumo wa mashine za Biometric Voter Registration (BVR), wajitokeze kujiandikisha kwasababu zoezi hilo mwisho leo

MKUU wa Mkoa wa Arusha Daud Ntibenda

Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusiana na mwisho wa zoezi hilo alilosema lilianza rasmi Mkoani Arusha Julai 6 mwaka huu, amesema ni vema wananchi wakatumia muda wa siku moja kujiandikisha.

Amesema Mkoa wa Arusha ulitarajia kuandikisha wapiga kura 980,000 kwenye jumla ya vituo 1,446 ambavyo vipo ndani ya mkoa mzima wa Arusha, hata hivyo watavuka lengo la idadi hiyo, kutokana na mwitikio ulivyo.

Amesema zoezi hilo lilipangwa kwa awamu nne na kila awamu ilikuwa na vituo 369, hivyo hadi kufikia awamu ya tatu ambayo imemalizika wiki iliyopita, mkoa umeweza kuandikisha asilimia 83.

Aidha amesema amepeleka ombi maalum kwa Tume ya Taifa ya uchaguzi kuongeza siku, kutokana na idadi ya watu kuwa kubwa hadi kufikia mwisho wa zoezi hilo, bado wananchi wanaonekana kuwa wengi hawajajiandikisha.

Hata hivyo amepiga marufuku kwa mtu yoyote nje ya mkuu wa mkoa, Katibu Tawala na kamanda wa polisi wenye mamlaka ya kutangaza kuhusiana na zoezi hilo, wengine wote waache kutoa matangazo ya kuwachanganya wananchi, vinginevyo hatua kali dhidi yao itachukuliwa.