Ijumaa , 3rd Jul , 2015

Uendelezaji wa utalii kwa siku za usoni na matumizi bora ya ardhi yatapatikana pale mipango bora ya maeneo ya hifadhi yanayopakana na makazi ya watu yatapangiliwa vizuri ili kuepukana na migogoro inayojitokeza baina ya wahifadhi na wananchi.

Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu katika mkutano kati ya wizara hiyo na jumuiya za hifadhi za wanyamapori (WMAS) uliofanyika jijini Arusha ambapo amesema ili kuwa na uhifadhi endelevu utakaorithiwa na vizazi vijavyo mpango wa matumizi bora ya ardhi hauna budi kuzingatiwa

Awali akizungumza mwenyekiti wa chama cha waongoza watalii nchini Wilbard Chambulo amesema kuwa ili uhifadhi uweze kufanikiwa lazima wanakijiji wawe na hati miliki za maliasili na pia serikali lazima iwape wananchi uhuru wa kupangilia mapato wanayopata kutokana na WMA, zao ili waweze kuzitunza vyema.

Tanzania ina jumla ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori (WMAS) 21 ambazo ni kilometa za mraba 36237.7 na jumuiya nyingine 17 ziko katika hatua mbalimbali za uanzishwaji.