Alhamisi , 2nd Jul , 2015

Nyota wa muziki na mjasiriamali mkubwa nchini Kenya, Jaguar hatimae amefanikiwa kukutana na kijana aliyekamatwa kwa kosa la kuruka ukuta wa Ikulu ya nchini Kenya, katika jaribio lake kwenda kukutana na rais wa nchi hiyo.

msanii wa muziki wa nchini Kenya jaguar akiongea na kijana anayehitaji msaada

Jaribio hilo la kuruka ukuta kwa kijana huyo limefahamika baadae kuwa alimtaka Rais amsaidie kufanikisha ndoto zake kufanya muziki.

Jaguar ambaye kwa sasa anafanya vizuri na rekodi yake mpya ya barua kwa Rais, ameeleza kuwa kwa kuanzia atamsaidia kijana huyo ambaye anafahamika kwa jina Mathew Kinuthia kujiendeleza kielimu kwanza ambapo atamlipia ada, na pia kumsaidia kufanya muziki kutimiza malengo yake.

Staa huyo ameeleza kuwa, Kinuthia anahitaji kurejea shule baada ya kuacha masomo akiwa kidato cha kwanza kwa kukosa ada, akiwa tayari kwa jitihada binafsi na wimbo mmoja wa asili ya kabila ya Kikuyu huko Kenya unaofahamika kwa jina Jubiree.