Jumanne , 30th Jun , 2015

Jumla ya 18,751 ya wanafunzi waliofanya mitihani ya kidato cha nne, mwaka jana wamekosa nafasi za masomo za kujiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi kutokana na sababu mbalimbali.

Jumla ya wanafunzi 18,751 kati ya wanafunzi 73,754 waliofaulu mitihani ya kidato cha nne, mwaka jana wamekosa nafasi za masomo za kujiunga kidato cha tano na vyuo vya ufundi kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumza jijini Dar es salaam Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kassim Majaliwa, amesema wanafunzi 55,003 sawa na asilimia 74.54 ya waliofaulu, wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano na mafunzo ya ufundi mwaka huu, kati yao wavulana ni 31,700 na wasishana ni 23,303 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 918 ikilinganishwa na wanafunzi 54,085 waliochaguliwa mwaka jana.

Majaliwa ametaja sababu za wanafunzi hao kutochaguliwa kuwa ni pamoja na ufinyu wa nafasi za shule , kushindwa kupata tahasusi, umri mkubwa wa watahiniwa wa kujitegemea pamoja na kukosa sifa za kuchaguliwa.

Akitaja mgawanyo wa wanafunzi waliochaguliwa amesema wanafunzi 29,744 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya sayansi na hisabati wakiwamo wavulana 18,294 na wasichana 11,450 sawa na asilimia 54.08.

Pia, alisema wanafunzi 25,259 wakiwamo wavulana 13,406 na wasichana 11,853(45.92) wamechaguliwa kujiunga na masomo ya Sanaa na Biashara.

Aidha Majaliwa ameongeza kuwa muhula wa kwanza kwa masomo ya kidato cha tano mwaka huu, utaanza Julai 18 na kuwataka wanafunzi kuripoti katika shule walizopangiwa kwa wakati na kwamba watakaoshindwa kuripoti shuleni zaidi ya siku 14 nafasi zao zitachukuliwa na wanafunzi ambao wamekosa nafasi.

Hata hivyo amesisistiza kuwa wanafunzi hao watadahiliwa na Baraza la Taifa la Ufundi (NACTE) kwenye fani mbalimbali zikiwamo za ualimu, afya, maendeleo ya jamii na kilimo.