Jumapili , 7th Jun , 2015

Timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inaweza kucheza mchezo mmoja wa kirafiki nchini Ethiopia kabla ya kwenda kumenyana na Misri wiki ijayo, mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika.

Stars ambayo imeweka kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia inajiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017 dhidi ya timu ya taifa ya Misri.

Na Chama cha Soka cha Ethiopia (EFF) kinaangalia uwezekano wa Taifa Stars kupata mchezo mmoja wa kirafiki wa kujipima nguvu kabla ya kuelekea nchini Misri.

Daktari wa Taifa Stars, Billy Haonga amesema hali ya hewa ya Addis Ababa ni nzuri kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Misri, kutokana na timu kufanya mazoezi katika ukanda wa juu ambao ni mwinuko kutoka usawa wa bahari hali itakayopelekea wachezaji kuwa fiti kwa ajili ya mchezo.

Haonga amesema, hali ya hewa ya Alexandria ni ya kawaida, hakuna baridi sana kutokana na kuzungukwa na bahari ya la Mediterania, hivyo kipindi cha wiki moja watakachokuwa kambini wanatarajiwa vijana watakuwa vizuri kabisa kwa ajili ya mchezo huku wachezaji hao wakiwa katika hali nzuri, kiafya, kifikra na morali ya juu kujiandaa na mchezo dhidi ya ‘Mafarao’.