Alhamisi , 24th Aug , 2023

Kocha Mkuu wa Azam FC, Yossouf Dabo, ameahidi kupindua meza katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Bahir Dar Kenema ya Ethiopia.

Akizungumza jijini Dar es salaam, kocha huyo amesema wachezaji wake walipoteza umakini na kufanya makosa madogo yaliyoigharimu timu hiyo katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa ugenini, hivyo wamerejea kwenye uwanja wa mazoezi kufanyia marekebisho mapungufu hayo.

“Yalikuwa ni matokeo ya kushangaza kwetu, tulikutana na mpinzani ambaye yupo imara kuliko tulivyofikiria, bado tuna nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata. Tumerudi nyumbani kufanyia kazi upungufu wetu,” amesema Dabo.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa mwishoni mwa juma lililopita kwenye Uwanja wa Abebe Bilkila, Ethiopia, Azam FC ilifungwa mabao 2-1, hivyo kesho ljumaa (Agosti 25) katika mchezo wa mkondo wa Pili, itahitaji ushindi wa bao l-0 pale Uwanja wa Azam Complex, Dar ili kufuzu hatua ya kwanza ya michuano hiyo.

Mshindi wa jumla kati ya Azam FC na Bahir Dar Kenema anatarajia kukutana na Club Africain ya Tunisia katika hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.