Jumapili , 29th Mei , 2016

Kocha Mkuu wa Real Madrid Mfaransa Zinedine Zidane ambaye enzi zake alijulikana kama 'Zizou' ameweka rekodi tatu kubwa huku pia akiweka rekodi ya kipekee yakuwa Mfaransa wa kwanza kuchukuwa ubingwa huo akiwa kocha wa timu ya nje ya nchi yake.

Kocha Mkuu wa Real Madrid akiwa na kombe la klabu bingwa Ulaya walilotwaa jana usiku.

Timu ya soka ya Real Madrid imewachapa mahasimu wao wa Jiji moja la Madrid, timu ya Atletico Madrid kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo mgumu mno wa fainali ya ligi a mabingwa barani Ulaya mchezo uliodumu kwa dakika 120.

Katika mchezo huo kocha mkuu wa Real Madrid Zinedine Zidane ameweza kuweka rekodi ya aina yake tatu tofauti ambazo hazijawahi kufikiwa na mtu mwingine.

Miongoni mwa rekodi hizo ni pamoja na kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid raia wa Ufaransa ni kushinda kombe hilo akiwa kama mchezaji, pili akiwa kama kocha msaidizi na sasa akishinda kwa mara nyingine akiwa kama kocha mkuu wa timu hiyo.

Penati muhimu kabisa ya mwisho iliyowapa ubingwa wa 11 wa kombe hilo Real Madrid iliwekwa kimiani kiufundi na mshambuliaji kipenzi cha Zidane, Mreno Cristiano Ronaldo.

Baada ya kuweka rekodi hizo tatu kwa mpigo ndani ya Real Madrid Zinedine Zidane jana usiku akiwa na furaha kubwa akatamka kuwa klabu hiyo ndiyo timu yake ya maisha.

Ikumbukwe katika uchezaji wake kiungo huyo fundi wa zamani wa Real Madrid na Ufaransa mwenye asili ya Afrika [ Algeria] aliwafungia Madrid goli ambalo liliwapa ubingwa wa Ulaya kwa mara ya tisa.

Na pia namba mbili akiwa msaidizi wa kocha Carlo Ancelotti wakati huo wakitwaa ubingwa huo kwa mara ya 10 na sasa ametwaa ubingwa huo tena kwa mara ya 11 akiwa kocha mkuu wa timu hiyo.

Zidane amemalizia kwa kusema kwa furaha "klabu hii ni ya maisha yangu imenipa nafasi ya kufanya kila kitu, nilipokuwa nafundisha timu B nikafuatwa na kuambiwa natakiwa kukabidhiwa timu ya kwanza nashukuru nilijiamini nitaweza nikapewa nafasi na sasa nimefikia hapa nikiwa kocha mkuu wa timu hii ambayo naipenda sana".