Jumamosi , 12th Dec , 2015

Ule msemo unaosema 'usiyempenda kaja' umeendelea kuliandama soka la Tanzania kimataifa mara baada ya timu za Tanzania kuendelea kupangwa kukutana na timu za warabu katika michuano ya CAF kwa vilabu barani Afrika, klabu bingwa na kombe la shirikisho.

Kikosi cha Yanga ambacho kitaiwakilisha Tanzania katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika mwakani.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, Yanga SC wataanza na Cercle de Joachim ya Mauritius katika Raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, wakati Azam FC itaanzia Raundi ya Kwanza.

Azam FC itakutana na mshindi kati Bidvest Wits ya Afrika Kusini na wawakilishi wa Shelisheli ambao hawajapatikana.

Yanga itaanzia nyumbani kati Februari 12, 13 na 14 mwakani huku ikimalizia ugenini kati ya Februari 26, 27 na 28 na ikivuka hatua hiyo, itakutana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Na kama ikivuka tena hatua hiyo, itakutana na Al Ahly ya Misri, au mshindi kati ya Recreativo de Libolo ya Angola na Racing Micomiseng ya Equatorial Guinea.

Azam FC itaanzia kucheza ugenini kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kumalizia nyumbani kati ya Machi 18, 19 na 20 na ikivuka mtihani huo, itakutana na ama Esperance ya Tunisia, wawakilishi wa Chad au News Stars de Douala ya Cameroon.

Mabingwa wa Zanzibar, Mafunzo wataanzia Raundi ya awali na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wakati JKU itacheza na Gaborone ya Botswana katika Kombe la shirikisho.