Kikosi cha timu ya Yanga katika moja ya michezo yake kikiingia katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Yanga wamesema bado hawajakata tamaa ya kutetea ubingwa wa ligi hiyo ambayo sasa inaongozwa na Azam Fc inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza msimu huu.
Afisa habari wa timu hiyo Baraka Kizuguto amewataka mashabiki wa timu hiyo kuiunga mkono timu yao kwakua bado wana michezo minne mkononi na kesho wanauhakika wa kuibwaga JKT Ruvu katika mchezo utakaopigwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Aidha Kizuguto amekanusha habari kuwa baadhi ya nyota wa timu hiyo ambao hawako kambini kujiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya JKT Ruvu kwamba wametimuliwa baada ya kutuhumiwa kuihujumu timu hiyo
Kwa upande mwingine klabu ya soka ya Yanga imeliandikia barua shirikisho la soka nchini TFF kutaka wapewe pointi 3 za mchezo wao dhidi ya Mgambo Shooting uliofanyika jijini Tanga na timu hiyo kuchapwa mabao 2-1 na maafande hao wa Tanga.
Afisa habari wa timu hiyo Baraka Kizuguto amesema kuwa sababu za kupeleka malalamiko yao TFF ni kutokana na timu ya Mgambo Shooting kumchezesha mchezaji Mohamed Husein Neto ambaye usajili wake haujakamilika kwakua ni raia wa kigeni na hivyo baada ya kujiridhisha na hilo wameamua kuandika barua hiyo ya malalamiko TFF.