Jumatano , 29th Aug , 2018

Klabu ya Yanga imeeleza juu ya mipango yake kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda hii leo kuwa inataka kushinda ili kuweka morali katika kundi hilo.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera (kushoto) na Nahodha, Gadiel Michael.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari mjini Kigali kuelekea mchezo huo, kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema .

Tunataka kuendeleza wimbi letu la ushindi, tunajua kuwa ndoto yetu imeshayeyuka katika mashindano haya lakini ushindi dhidi ya Rayon Sports utatusaidia kuimarisha hari yetu ya ushindi na kuleta morali katika kundi hili. Lengo letu kubwa kwa sasa ni kushinda ubingwa wa ligi “.

Naye nahodha wa kikosi cha Yanga kitakachoanza katika mchezo huo, Gadiel Michael amesema kuwa hari ya wachezaji ni kubwa kuelekea mchezo huo na kwamba wamekwenda mjini Kigali kwaajili ya kufanya kazi moja tu ya kuhakikisha wanamaliza mchezo wa mwisho kwa kuacha historia nzuri ya michuano hiyo.

Yanga inakamata nafasi ya mwisho katika kundi lao ikiwa na alama nne ikifuatiwa na Rayon Sports yenye alama 5 ambapo timu zote zimeshindwa kufuzu hatua inayofuata ya michuano hiyo. Endapo Yanga itashinda mchezo wa leo itafikisha alama saba ambazo ni alama moja nyuma ya USM Alger yenye alama nane kabla ya mchezo wa mwisho.

Gor Mahia ya Kenya inaongoza kundi hilo kwa alama nane, itacheza mchezo wa mwisho dhidi ya USM Alger huku timu zote zikiwa zimeshajihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.