Ijumaa , 24th Jul , 2015

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Soka Tanzania Bara Young African imeiondoa timu ya KMKM katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuichapa bao 2-0 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Yanga ilianza kujipatia goli lake la kwanza katika kipindi cha pili dakika ya 56 kupitia kwa mshambuliaji wake Malimi Busungu huku bao la pili likifungwa katika dakika ya 72 kupitia kwa mshambuliaji wake Amisi Tambwe aliyetokea benchi akichukua nafasi ya Busungu.

Kwa mchezo huo, Busungu anatimiza magoli matatu katika michuano hiyo baada kuichapa Telecom bao 3-0 Busungu akitupia bao mbili nyavuni.

Katika mchezo wa awali Khartoum imetoshana nguvu na Gor Mahia baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na kupelekea Khartoum kuendelea kuongoza kundi A kwa kuwa na Pointi saba sawa na Gor Mahia wakiwa na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa ikifuatiwa na Yanga yenye pointi sita, KMKM yenye Pointi tatu na Telecom ambayo haina pointi hata moja.