Kiungo Justine Zulu wa Yanga akiwa chini baada ya kufanyiwa madhambi
Taarifa hiyo ni baada ya klabu hiyo kupokea taarifa kutoka kwa daktari wa kikosi hicho Dkt. Edward Bavu zinazoonesha kuwa mchezaji huyo ataweza kuendelea na mechi zilizobaki kwa kuwa hakuvunjika mfupa wa mguu.
Dkt. Bavu amesema licha ya kiungo huyo kuonekana kuumizwa sana na kiungo wa Azam FC, Himid Mao hali iliyopelekea kushonwa nyuzi tisa, jeraha lake halijahusisha viungo, hivyo anaweza kuwahi kurejea dimbani kuliko vile walivyotoa taarifa awali.
"Unajua aliumia kwa kuchubuliwa ngozi na si kuvunjwa mfupa, ingekuwa hivyo kupona kwake kungechukua muda kidogo lakini hivi anaweza kupona haraka kwani ni jereha tu la kidonda likipona hili na maumivu kuisha basi atarajea mapema zaidi, tofauti na vile tulivyosema mwanzoni". Alisema Bavu katika taarifa yake kwenda kwa Klabu ya Yanga SC

Dkt. Bavu
Awali klabu hiyo ilisema Zulu angeweza kukaa nje ya dimba kwa zaidi ya siku 14 lakini sasa matumaini kwa wanayanga yanaanza kurejea kwa kasi kutokana na mchango wake kuelekea Michuano ya Shirikisho la Soka Barani Afrika pamoja na Ligi kuu ambayo mpaka sasa wao ndiyo wapo kileleni.

