
Mchezaji Elisha Muroiwa
Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga ameongea na East Africa Radio na kuweka wazi kuwa ni kweli wamempokea mlinzi huyo wa kati wa timu ya taifa ya Zimbabwe baada ya Yanga kusema hawana mahitaji naye tena licha ya awali kueleza kuhitaji huduma ya nyota huyo kwaajili ya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.
''Elisha ni mchezaji wetu kwasasa, makubaliano ya awali ya viongozi wa Yanga na Singida United alitakiwa ajiunge na Yanga kwa msimu ujao, baada ya viongozi wao kusema kunaupungufu wa beki kwenye kikosi hususani kwa kipindi hiki cha kombe la shirikisho na ligi msimu ujao lakini sasa wamemrudisha nasi tumempokea'', - amesema.
Sanga ameongeza walipokea taarifa ya Yanga kumkataa Elisha dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili kufungwa na wao walifanya taratibu haraka wakakamilisha usajili wake hivyo ataitumikia Singida United kwa miaka miwili.
Yanga ilifanikiwa kumuongeza mkataba mlinzi wake Kelvin Yondani jana usiku baada ya kuwa kwenye maongezi kwa muda mrefu tangu mkataba wake umalizike mapema mwezi Mei. Kwa kumalizana na Yondani Yanga wakaona tena hawahitaji huduma ya Muroiwa na wakachukua uamzi wa kumrejesha Singida United.