Jumamosi , 9th Apr , 2016

Baada ya wawania ubingwa wenzao timu ya Azam FC kushuhudiwa ikishindwa kula viporo vyao viwili vya awali kati ya vitatu, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania bara Yanga SC nao wameanza kuingiwa na hofu ya huenda nao wakakumbana na kadhia hiyo.

Kikosi cha timu ya Yanga SC.

Klabu ya soka ya Yanga baada yakushuhudia wenzao Azam FC wakishindwa kula viporo vyao viwili baada ya kuchacha nao Yanga ambao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara wameanza kuingiwa na hofu ya kuwa huenda nao viporo vyao vikachacha na hivyo kuwapa mwanya vinara wa ligi hiyo kwa sasa watani wao wa jadi Simba SC kuendelea kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo.

Azam FC wameshindwa kula viporo vyao baada ya kushindwa kuibuka na ushindi katika michezo yao miwili ya viporo kati ya mitatu waliyokuwa nayo ambapo timu hiyo ilianza kwa sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Toto Africans wanakishamapanda kutoka Jijini Mwanza.

Kiporo kingine cha Azam FC kilichacha nyumbani katika uwanja wao wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es Salaam baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na wanakuchele Ndanda FC ya Mtwara hali ambayo imewatisha Yanga na kuanza kujiuliza mara mbili mbili wavitafunaje viporo vyao viwili vilivyobaki.

Licha ya Yanga kupata ushindi katika moja ya viporo vyao vitatu walipoibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam lakini bado wanawasiwasi huenda wakakutana na hali ngumu kwenye michezo miwili ijayo ya viporo na hivyo kuwaacha wapinzani wao Simba kuendelea kujiwekea mazingira mazuri yakutwaa ubingwa.

Hofu ya timu ya Yanga iko katika mambo mawili kwanza mchezo wake wa pili wa kiporo itakutana na timu ngumu na isiyotabirika ya Mtibwa Sugar pamoja na mchezo huo kuchezwa katika uwanja wa taifa lakini kwa hali ilivyo lolote linaweza kutokea katika mchezo huo.

Na jambo lingine linalowapa hofu Yanga na kuwapa wakati mgumu ni kwamba michezo yao mingi iliyobakia watacheza nje ya Dar es Salaam yaani ugenini katika viwanja vya mikoani ambavyo mara nyingi vimekuwa sio rafiki kwa timu hiyo na kuwapa taabu sana wachezaji kucheza mpira wao hasa kutokana na ubovu wa dimba la kuchezea na hivyo pengine ikawa fursa ya wapinzani wao wa jadi timu ya Simba wanaoongoza ligi hiyo kwa alama 57 kuendelea kung'ang'ania kileleni hasa ikizingatiwa michezo yao mingi wataichezea katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Michezo ambayo timu ya Simba itakuwa nje ya Dar es Salaam ni miwili dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa mjini Morogoro katika uwanja wa Jamhuri na ule dhidi ya wanalizombe Majimaji FC utakaopigwa katika dimba la Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.