
Mlinzi wa kati wa Simba, Joash Onyango (kushoto) na Taddeo Lwanga (kulia) wakifanya mazoezi kabla ya kuwavaa Dodoma Jiji.
Kuelekea kwenye mchezo huo, Simba imethibitisha kurejea kikosini kwa wachezaji wake watatu nyota waliopata majeraha kwenye mchezo wake uliopita wa michuano ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Wachezaji hao waliorejea ni mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe, kiungo, Taddeo Lwanga na mlinzi wa kati, Joash Onyango ambapo Kapombe na Lwanga wamezungumza kuelekea mchezo huo.
Kapombe amesema “Tunaomba mashabiki wote wa Simbaa waweze kujitokeza kwa nguvu kutuunga mkono, tunajua sisi ni wao na wao ni sisi, watuunge mkono ili tuweze kufanya vizuri na kutinga hatua inayofuata”.
Kwa upande mwingine, kiungo Taddeo Lwanga amesema wanasimba wajitokeze kwa wingi kwani wanazawadi yao. “Tuna zawadi kwa ajili yenu, mjitokeze kwa wingi”.
Naye kocha wa klabu ya Dodoma Jiji, Mbwana Makata amesema wamejifunza baada ya kucheza michezo miwili ya Ligi kuu dhidi ya Simba na kupoteza michezo yote, mmoja wakifungwa 2-1 na wa mwisho kukutana Aprili 27, 2021 kwa mabao 3-1.
“Tutaingia kwa nidhamu yote kwa kujua tunacheza na timu iliyokuwa bora ili kuhakikisha tunaweza kupata matokeo kwenye mchezo huo. Nashukuru pia vijana wangu wameshaiona Simba na wameshacheza nayo Dodoma wakatufunga 2-1 na mechi ya pili tulicheza nao kwenye uwanja tutakaocheza nao leo na walitufunga mabao 3-1”.
“Kuba vingi vya kujifunza, kuna makosa tuliyafanya inabidi tuyarekebishe”. Akamalizia Makata.
Uongozi wa klabu hiyo pia imeahidikutoa zawadi ya donge nono kama kikosi hicho kitafanikiwa kuitoa Simba ambao ni mabingwa watetezi.
Mshindi wa mchezo huo atacheza na Mshindi kati ya Azam na Rhino Rangers ilhali Yanga atacheza na Biashara United Mara kwenye mchezo wa nusu fainali.