Jumanne , 6th Nov , 2018

Klabu ya soka ya Mtibwa Sugar kupitia kwa msemaji wake Thobias Kifaru, imejinadi kuwa mchezo wao wa leo dhidi ya Alliance FC utakuwa rahisi sana kwani timu hizo mbili ni za madaraja mawili tofauti, wao wakiwa ni Chuo Kikuu cha soka Tanzania na Alliance ni wanafunzi wa msingi.

Juu ni Alliance FC na chini ni Mtibwa Sugar

Kifaru amedai kuwa kutokana na matokeo ya mechi zao mbili za nyuma ambapo wameshinda dhidi ya Kagera Sugar pamoja na Ruvu Shooting hivyo haoni kama timu changa ya Alliance itawazuia.

''Tunakwenda kucheza na wanafunzi wa darasa la sita sisi ni chuo kikuu cha soka Tanzania hilo liko wazi kwahiyo tumekomaa na hakuna namna yoyote ya kutuzuia kuchukua pointi tatu muhimu'', amesema.

Mtibwa Sugar tayari ipo Mwanza kwaajili ya mchezo huo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Nyamaghana kuanzia saa 10:00 jioni ambapo vijana wa shule ya soka ya Alliance watakuwa wanajaribu kujikwamua kutoka katika nafasi za chini za msimamo wa ligi.

Alliance wanashika nafasi ya 18 wakiwa na alama 10 kwenye mechi 13 huku Mtibwa Sugar wakiwa nafasi ya 4 wakiwa na alama 23 kwenye mechi 13 walizocheza mpaka sasa.