Jumatatu , 12th Aug , 2019

Klabu ya soka ya Azam FC imeweka wazi kuwa inajipanga kwaajili ya mchezo wa marudiano na Fasil Kenema ya Ethiopia ili kuhakikisha inapata ushindi na kusonga mbele baada ya kufungwa 1-0 ugenini.

''Dakika 90 za kwanza zimemalizika ugenini, sasa tunajipanga vilivyo kumalizia vita ya dakika 90 nyingine nyumbani na kupata matokeo bora yatakayotufanya tusonge mbele kwa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika'', imeeleza taarifa ya Azam.

Azam FC ni miongoni mwa vilabu vinne vya Tanzania vinavyowakilisha nchi kwenye michuano ya Afrika ngazi ya vilabu.

Azam FC na KMC zinawakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo KMC siku ya Jumamosi ilicheza na AS Kigali huko Rwanda na kutoka suluhu.

Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika Tanzania inawakilishwa na Yanga ambao walitoka sare ya 1-1 na Township Rollers pamoja na Simba ambao walitoka suluhu na UD Songo ya Msumbiji.