Jumapili , 11th Aug , 2019

Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera amesema kuwa wachezaji wake wanakosa maelewano mazuri uwanjani, sababu inayopelekea kutopata matokeo kwenye mechi kubwa.

Mchezo wa Yanga na Township Rollers

Amezungumza hayo baada ya kumalizika kwa mchezo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana katika Uwanja wa Taifa, na kushuhudia sare ya bao 1-1.

"Wachezaji wangu bado wanasumbuliwa na tatizo la kushindwa kuelewana wakiwa ndani ya uwanja jambo ambalo linaleta ugumu kwenye kupata matokeo uwanjani", amesema kocha Zahera.

"Kwa sasa hesabu ni kuona kwamba tunakuwa na kikosi imara ambacho kitapata matokeo kwenye mchezo wetu wa marudio, mashabiki waendelee kutupa sapoti katika hili, nami nitafanyia kazi makosa yote. Tuna imani ya kupata magoli mechi ijayo, naamini tuna uwezo huo", ameongeza.

Yanga inatarajia kusafiri nchini Botswana ambapo itacheza mchezo wa marudiano na Township Rollers mnamo Agosti 23-25. Itahitaji kupata sare ya magoli mawili au kushinda kwa idadi yoyote ya magoli ili kuweza kusonga mbele.