Ijumaa , 2nd Jul , 2021

Mchezo wa watani wa jadi kutoka mitaa ya kariakoo 'Kariako Derby' unaozikutanisjha timu za Simba na Yanga, unataraji kuchezwa kesho saa 11:00 jioni kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam baada ya mchezo huo kughairishwa Mei 8 mwaka huu.

Mlinda mlango wa Yanga, Metacha Mnata (kushoto) na kiungo wa Simba, Jonas Mkude (kulia).

Kulelekea kwenye mchezo huo ambao Simba itakuwa mwenyeji, Wekundu hao wa msimbazi wanataraji kuwakosa wachezaji wake watatu kutokana na sababu mbali mbali.

Wachezaji watakaokosekana kesho Jumamosi Julai 3, 2021 ni winga mzimbabwe, Perfect Chikwende aliyepo kwenye majukumu ya timu ya taifa, Ibrahim Ajib ambaye hayupo kikosini na kiungo wake wa muda mrefu, Jonas Mkude aliyesimamishwa kutokana na sababu za utovu wa nidhamu.

Licha ya kukosekana kwenye mchezo huo, huenda kocha wa Simba, Mfaransa Didier Gomez Da Rosa asiumize kichwa kwani tokea nyota huyo ajiunge na Simba kwenye dirisha dogo mwaka huu hajaweza kucheza michezo mingi na badala yake ameambulia benchi kwenye michezo ya ligi kuu pekee.

Kwa upande wa Ibrahim Ajib, pia ameshindwa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza tokea ajiunge wa mabingwa hao watetezi wa VPL misimu miwili iliyopita akitokea kwa watani wake wa jadi, Yanga.

Mkude ambaye ameandamwa na masuala ya kinidhamu amepoteza nafasi kwenye kikosi cha Simba tokea mwezi Disemba mwaka jana aliposimamishwa na klabu yake kutokana masuala hayo hayo ya kinidhamu licha ya kurejea kikosini mwezi Machi lakini akajikuta anasimamishwa tena mwezi mei.

Simba huenda ikaendelea kumtumia winga wake, Bernard Morrison kucheza nafasi ya Chikwende, kiungo mganda, Taddeo Lwanga kucheza nafasi ya Mkude ilhali Larry Bwalya kucheza nafasi ya Ibrahim Ajib kama ambavyo wamekuwa wakicheza na kuonesha kiwango kizuri.

Kwa pande wa Yanga kupitia kwa meneja wa timu, Hafidh Salehe amesema, mlinzi wa kati, Lamine Moro, mshambuliaji Michael Sarpong wote kutoka taifa la Ghana na mlinda mlango mzawa, Metacha Mnata wote wakisimamishwa kutokana na masuala ya utovu wa nidhamu klabuni hapo.

Lamine Moro alisimamishwa na klabu hiyo takribani miezi iliyopita baada ya taarifa za awali kueleza nahodha huyo wa Yanga alipishana lugha na kocha wake Mohamed Nasrdeen Nabi na kuondolewa kambini wakati timu yake ilipokuwa inajiandaa kucheza dhidi ya Namungo kwenye VPL.

Michael Sarpong amesimamishwa kwa utovu wa nidhamu bila ya suala lake kuwekwa wazi lakini Metacha anaendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu na bodi ya Ligi baada ya kuwatukana mashabiki kwa ishara baada ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting kumalizika.

Yanga huenda ikaendelea kuwatumia Dickson Job kuchukua nafasi ya mlinzi wa kati, Lamine Moro, Fiston Abdulrazak kuchukua nafasi ya Michael Sarpong na mlinda mlango Farouk Shikhalo kuchukua nafasi ya Metacha Mnata kama ambavyo wamecheza kwenye michezo iliyopita na kuonesha ubora.